Matthew 9

Isa Amponya Mtu Aliyepooza

(Marko 2:1-12; Luka 5:17-26)

1 aIsa akaingia kwenye chombo, akavuka na kufika katika mji wa kwao. 2 bWakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Isa alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa.”

3 cKwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa sheria wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!”

4 dLakini Isa akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu? 5Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 6 eLakini, ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” 7Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani kwake. 8 fMakutano walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu ambaye alikuwa ametoa mamlaka kama haya kwa wanadamu.

Kuitwa Kwa Mathayo

(Marko 2:13-17; Luka 5:27-32)

9 gIsa alipokuwa akienda kutoka huko, alimwona mtu mmoja jina lake Mathayo akiwa ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Isa akamwambia, “Nifuate.” Mathayo akaondoka, akamfuata.

10Isa alipokuwa akila chakula ndani ya nyumba ya Mathayo, watoza ushuru wengi na “wenye dhambi” wakaja kula pamoja naye na wanafunzi wake. 11 hMafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”

12Lakini Isa aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu. 13 iNendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

Isa Aulizwa Kuhusu Kufunga

(Marko 2:18-22; Luka 5:33-39)

14 jWanafunzi wa Yahya Mbatizaji wakaja na kumuuliza Isa, “Imekuwaje kwamba sisi na Mafarisayo tunafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”

15 kIsa akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kuomboleza wakati angali pamoja nao? Wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.

16 l“Hakuna mtu anayeshonea kiraka kipya kwenye nguo iliyochakaa, kwa maana kile kiraka kitachanika kutoka kwenye hiyo nguo, nayo hiyo nguo itachanika zaidi. 17Wala watu hawaweki divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Kama wakifanya hivyo, viriba vitapasuka nayo divai itamwagika, navyo viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya, na hivyo divai na viriba huwa salama.”

Mwanamke Aponywa

(Marko 5:21-43; Luka 8:40-56)

18 mIsa alipokuwa akiwaambia mambo haya, mara akaingia kiongozi wa sinagogi akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye atakuwa hai.” 19Isa akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye.

20 nWakati huo huo, mwanamke mmoja, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaja nyuma ya Isa, akagusa upindo wa vazi lake, 21 okwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.”

22 pIsa akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo mkuu, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa ile ile.

Isa Amfufua Binti Wa Kiongozi Wa Sinagogi

23 qIsa alipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, 24 rakawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. 25 sLakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. 26 tHabari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.

Isa Awaponya Vipofu

27 uIsa alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipiga kelele kwa nguvu na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!”

28 vAlipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Isa akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?”

Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”

29 wNdipo Isa akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.” 30 xMacho yao yakafunguka. Isa akawaonya vikali, akisema, “Angalieni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.” 31 yLakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.

Isa Amponya Mtu Bubu

32 zWalipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Isa. 33 aaYule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea. Ule umati wa watu ukastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.”

34 abLakini Mafarisayo wakasema, “Huyo anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa mkuu wa pepo wachafu.”

Watendakazi Ni Wachache

35 acIsa akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi. 36 adAlipoona makutano, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. 37 aeNdipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. 38 afKwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.”
Copyright information for SwhKC